Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma amewatahadharisha vijana wanaojikita katika kufanya kazi za kuajiriwa katika ofisi mbalimbali kuwa mafanikio halisi kwao itakuwa ndoto za alinacha.
Msukuma ambaye ni mmoja kati ya wafanyabiashara maarufu waliogeuka kuwa wanasiasa machachari na wenye ushawishi mkubwa, amesema kuwa anawashauri vijana wa Kitanzania kuachana na mawazo ya kutegemea kazi za kuajiriwa ofisini kwani haziwezi kuwapa mafanikio wanayoyaota bali zitawafanya wawe wametingwa tu.
“Tatizo la vijana wengi wa Tanzania wanatamani kuanzia kazi za maofisini. Lakini mimi nachokwambia ni kwamba kazi za ofisini haziwezi kukufanya mtu ukaendelea, inaku-keep tu busy (inakufanya uwe umetingwa),” alisema Mbunge huyo.
Alifafanua kuwa vijana wanapaswa kufahamu kuwa kazi nzuri na itakayowaletea mafanikio ni ile inayotokana na mawazo mbadala.
Alitoa mfano wa shindano la mawazo ya biashara lililokuwa linaratibiwa na Dkt. Reginald Mengi akitoa Sh10 milioni kwa washindi, alkieleza kuwa anaamini mfanyabiashara huyo atayafanyia kazi hata mawazo ambayo hayakufanikiwa kupata ushindi na baadaye watu watajionea.
“Kazi inayokufanya wewe kuwa na mawazo yako mbadala ni kazi muhimu sana. Ni kama anavyofanya Dkt. Reginald Mengi, kwamba unawaambia vijana niandikieni mawazo nawapa zawadi milioni 10. Lakini mawazo mengine yaliyofeli anawapa timu yake kwa ajili ya kuyafanyia kazi na mwisho wa siku utakuja kushangaa kitachotokea,” aliiambia Clouds Media.
Akizungumzia siri ya mafanikio yake kama mfanyabiashara mkubwa, alisema kuwa alianza kufanya biashara tangu miaka ya 1980, hivyo kujiwekea akiba pamoja na kukopesheka vimemfanya aweze kufikia kiwango alichofikia sasa kibiashara.