Wananchi nchini Msumbiji, wanapiga kura leo katika uchaguzi mkuu, kuchagua Rais wa nchi hiyo na Wabunge ambao wataendesha nchi kwa miaka mitano ijayo.
Nchi hiyo ya Kusini mashariki mwa Afrika, inafanya uchaguzi huu baada ya miezi miwili ya kusaini mkataba wa amani kati ya serikali na waasi wa Renamo.
Chama cha Msururu wa ukombozi wa Msumbiji (Frelimo) kinachoongozwa na Rais Filipe Nyusi, kinachuana vikali na chama cha upinzani wa kitaifa wa Msumbiji (Renamo) kinachoongozwa na Ossufo Momade.
Kampeni za uchaguzi huo ziliisha jana, ambapo wasiwasi wa usalama uliibuka baada ya mashambulizi ya silaha na matukio ya kigaidi katika sehemu za kaskazini mwa nchi hiyo, ambazo zina akiba ya gesi asilia.
Wagombea wengine wa urais ni Daviz Simango wa chama cha Demokrasia cha Msumbiji na Mario Albino wa chama cha AMUSI, ambacho kimeundwa na wale waliohama chama hicho.
Rais Nyusi anayetetea kiti chake, ameweka mbele hoja yake kwamba chama chake ni chama bora zaidi cha kuendesha nchi, wakati mgombea wa upinzaji Momade akiahidi kuboresha uchumi na kuongeza ajira.