Mshambuliaji Simon Msuva amepania kufanya makubwa kwenye mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika 2021 ‘AFCON’ utakaoshuhudia timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ wakicheza ugenini dhidi ya Equatorial Guinea, leo Alhamisi (Machi 25) majira ya saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Stars itakua ugenini mjini Malabo, ikiwa na lengo la kupata ushindi kwenye mchezo huo ili kufufua matumaini ya kuwa miongoni mwa timu zitakazofuzu fainali za Afrika 2021, zitakazofanyika nchini Cameroon.
Msuva anayeitumika klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco, amesema ana jukumu zito kwenye mchezo huo, ambao anatarajia utakua na ushindani mkubwa kutokana na hitaji lao la kuwapa raha watanzania.
Amesema kwa ujumla kikosi cha Taifa Stars ambacho kiliwasili mjini Malabo juzi Jumanne (Machi 23), kikitokea kambini mjini Nairobi, Kenya kipo kwenye hali nzuri na wachezaji wanahimizana kufanya kazi ya kupambana wakati wote watakapokua dimbani leo usiku.
“Tupo tayari kwa mapambano, naamini Watanzania wapo nyuma yetu hivyo hatutakuwa tayari kuwaangusha, nikiwa kama mchezaji ambaye ni sehemu ya timu nitapambana kwa kutoa mchango wangu wote ili kuhakikisha timu inapata kile ambacho tumekilenga, ushindi yatakuwa matokeo mazuri zaidi kwetu.” Amesema Msuva
Katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi hiyo, Tanzania ambayo ipo kundi J, inatakiwa kupata ushindi na ikishindikana ilazimishe sare ya aina yoyote dhidi ya Equatorial Guinea, ili kujiweka pazuri kabla ya kumalizia nyumbani, Tanzania mchezo wa hatua ya makundi dhidi ya Libya.
Stars inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi J ikiwa na alama 4, ikitanguliwa na Tunisia inayoongoza kundi hilo kwa kufikisha alama 10, Equatorial Guinea inashika nafasi ya pili kwa kumiliki alama 6 na Libya inaburuza mkia ikiwa na alama 3.