Kiungo Mshambuliaji kutoka Tanzania na Klabu ya Al-Qadsiah, Simon Msuva anapambana kuhakikisha anaikwamua timu hiyo isishuke daraja, kutokana na nafasi ya 15 iliopo sasa, huku ikiwa imebakiza mechi tatu tu kufunga msimu, huku akitaka kufunga mabao 15.
Katika michezo 21 iliyocheza timu hiyo, imeshinda mitano, sare saba, imepoteza tisa na imevuna alama 22, ina jumla ya mabao 15, huku Msuva akifunga saba katika michezo saba sawa na kusema kuwa amefunga nusu ya mabao yote.
Ili Al-Qadsiah isishuke daraja inatakiwa ishinde michezo mitatu iliyobakia, kwani timu tatu zilizopo chini yake ambazo ni Al Sahel ina alama 20, Najran ina alama 18 na Shoulla alama 11.
Msuva amesema anajiona ana kazi nzito ya kuitetea timu yake, hivyo anahitaji kufunga mabao mengi zaidi na ikiwezekana amalize na mabao 15 ambayo yatakuwa yakiipa ushindi wa kupata alama timu hiyo.
“Timu yangu haipo nafasi nzuri, hivyo naelekeza nguvu zangu, akili zangu zote nazipeleka hapa kuhakikisha nafunga mabao ya kupata pointi kwa maana timu ishinde na siyo sare ama kufungwa hiyo ndio itakuwa furaha yangu.
Ameongeza “Ndio maana natamani kufunga mabao mengi angalau nifikishe 15 kwa mechi zilizosalia, naamini kwenye dhamira hakuna kinachoshindikana na tabia yangu ni kutokukata tamaa kwa jambo lolote,” amesema mchezaji hiyo wa zamani wa Wydad Casablanca ya Morocco.
Amesisitiza hataki historia ya kushuka na timu, badala yake anatamani kuandika rekodi ya kukumbukwa huduma yake : “Natamani nifanye vitu vya kuacha alama kwamba alikuwepo Mtanzania alifanya kitu hiki kwenye timu, ndio maana naweka akili yangu kwenye hizo mechi tatu ili tubaki salama,” amesema.
Kabla ya kusajiliwa Al-Qadsiah, Msuva aliwahi kuzitumikia Difaâ El Jadida (2017-2020) na Wydad (2020-2022) na Tanzania alizichezea Azam FC (2010/11), Moro United (2011/12) na Young Africans (2012-2017).