Imefahamika kuwa Klabu ya JS Kabylie ya nchini Algeria itamlipa mshahara wa dola 25,000 (Sh mil 62.3) kwa mwezi mara baada ya kumsajili.
Msuva juzi Alhamis (Agosti 24) alifuzu vipimo vya afya JS Kabylie ambako amesaini mkataba wa miaka miwili na muda wowote kuanzia jana alitarajiwa kutambulishwa rasmi kama mchezaji wa timu hiyo inayovaa jezi za rangi ya njano na kijani.
Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka nchini Algeria kimesema, Msuva tayari amemalizana na JS Kabylie na watampa mshahara wa dola 25,000 kwa mwezi.
“Kila kitu kimeenda vizuri huku (Algeria) na Msuva alishafanyiwa vipimo vya afya na amefuzu tayari kwa kuanza kazi na wenzake. Kuhusu ishu ya mshahara atalipwa dola 25,000 kwa mwezi,” kimesema chanzo hicho cha kuaminika.
Msuva amejiunga na JS Kabylie kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake Al-Qadsiah FC ya Saudi Arabia.
Kabla ya hapo aliwahi kucheza Klabu za Wydad Casablanca, Difaá El Jadida, Yanga, Azam na Moro United.