Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu umaskini na haki za binadamu, Olivier De Schutter, amesema mataifa lazima yahakikishe kuwa mafao ya kijamii na mishahara vinapanda ili kuendana na mfumuko wa bei, ili kuepuka vifo vya ukali wa maisha.
De Schutter, ameyasema hayo na kuongeza kuwa kama ilivyokuwa wakati wa janga la Uviko-19, watu wa hali ya chini ambao wengi wao ni wanyonge ndiyo wanaoathirika zaidi kutokana na matukio yanayoikumba Dunia.
Amesema, mizozo katika maeneo mengi ulimwenguni inatarajiwa kupelekea watu milioni 75 hadi milioni 95katika umaskini uliokithiri kwa mwaka huu pekee (2022), na kwamba ili kupunguza tatizo hilo ni vyema wakuu wa nchi wakachukua hatua sahihi.
Aidha, De Schutter amelitaja bara la Ulaya ambako mfumuko wa bei umefikia rekodi ya juu ya asilimia 10, na kanda ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara, ambako bei za vyakula zimeongezeka kwa karibu asilimia 24.
Kufuatia hali hiyo, Mtaalamu huyo amezihimiza nchi kuwashirikisha watu wanaoishi katika umaskini katika kutunga sera zinazokusudiwa kukabiliana na gharama za maisha zinazopanda ili waweze kuchangia mawazo yao.
Amesema, ushiriki wa watu hao utakuwa ni kielelezo tosha cha kubainisha aina ya matatizo wanayokumbana nayo, na kwamba utengenezaji wa sera bila wao ni kujidanganya kwani wanaelewa fika adha wanazokutana nazo na njia za kukabili.