Imeelezwa kuwa, Shirika la Umeme Tanzania – TANESCO, litapeleka mtambo wa umeme wa MW 20 Mkoani Mtwara kutoka kituo cha umeme Ubungo III, ili kuimarisha hali ya umeme katika eneo hilo na Mkoa wa Lindi ikiwa ni utekelezaji wa agizo alilolitoa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko kwa TANESCO la kuimarisha hali ya umeme katika mikoa hiyo.
Hayo yamebainika wakati wa Kikao cha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko na Bodi pamoja na Menejimenti ya TANESCO kilichofanyika tarehe 21 Novemba, 2023 jijini Dodoma, kufuatia agizo la kuimarisha hali ya umeme katika Mikoa ya Lindi na Mtwara alilitoa wakati alipofanya ziara ya kikazi katika mikoa hiyo na kukuta hali isiyoridhisha ya upatikanaji umeme.
Aidha, Dkt. Biteko ameiagiza TANESCO kuongeza nguvu katika kutekeleza miradi ya uzalishaji umeme nchini kwa kutumia fedha zilizopo ili nchi iweze kuwa na umeme wa kutosha kusambazia wananchi ikiwemo umeme kutoka katika vyanzo vya nishati jadidifu.
Dkt .Biteko pia ameitaka Bodi ya TANESCO kulisimamia vyema Shirika hilo na wafanye kazi kwa kushirikiana na Menejimenti kwani lengo la Shirika hilo ni kuhakiksha kunakuwa na umeme wa kutosha kwa matumizi mbalimbali.
Aidha, amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-hanga kusimamia na kuwatumia Watendaji na Wataalam wa shirika hilo vizuri ili kuwe na ufanisi katika shughuli zao za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme.
Dkt. Biteko ameitaka TANESCO pia kuboresha Kitengo cha Huduma kwa Mteja kwa namna mbalimbali ikiwemo kuwaendeleza wataalam wanaotoa huduma kwa wananchi ili watoe huduma bora na yeye ameahidi kutoa ushirikiano kwa Shirika hilo pale utakapohitajika.
Dkt. Biteko pia, ameitaka Bodi ya TANESCO kutokuwa na urasimu katika ufanyaji wa maamuzi na uzito wa kufuatilia masuala mbalimbali ili kutochelewesha miradi mbalimbali ya umeme.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba ameitaka Menejimenti ya TANESCO kuwa wabunifu na kuongeza nguvu katika ufuatiliaji wa vitu mbalimbali ikiwemo miradi na pia kuongeza umakini na kasi katika utendaji kazi huku akieleza kuwa fedha za kutekeleza baadhi ya miradi hiyo zipo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Balozi, Meja Jenerali Paul Kisesa Simuli amempongeza Dkt. Biteko kwa kutoa miongozo mbalimbali ambayo inaendelea kuboresha utendaji kazi wa Shirika hilo na kueleza kuwa kikao hicho kimetoa njia ya wao kufanya kazi.
Aidha, ameahidi kutekeleza maagizo mbalimbali yaliyotolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, ikiwemo ya kuendeleza wataalam wanaofanya kazi katika Kitengo cha Huduma kwa Mteja.
Katika kikao hicho TANESCO imeeleza hatua mbalimbali wanazochukua ili kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme kwenye baadhi ya mikoa ikiwemo Dar es salaam hasa katika maeneo ya Temeke na Kinondoni ambako kuna ongezeko la mahitaji ya umeme na tayari hatua mbalimbali zitachukuliwa.
Hatua hizo ji pamoja na kuongeza uwezo wa miundombinu ya kusafirisha umeme kwa kujenga njia za kusafirisha umeme kutoka Kinyerezi hadi Mbagala kupitia Gongo la Mboto kwa ajili ya Wilaya ya Temeke hadi Mkuranga. Njia nyingine inayojengwa ni ya kusafirisha umeme kutoka Ubungo hadi Ununio ili kuimarisha upatikanaji umeme maeneo ya Mbezi Beach, Kunduchi na Mikocheni.