Mtambo wa kwanza wa kisasa wa kukausha nguzo za umeme katika nchi za Afrika Mashariki na Kati umezinduliwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani wilayani Mufindi Mkoa wa Iringa.
Hafla ya kuzindua mtambo huo umefanyika katika kiwanda cha nguzo cha Sao Hill kilichopo wilayani Mufindi kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Iringa wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Saad Mtambule na Mbunge wa Mafinga, Cosato Chumi.
Akitoa taarifa kuhusu mtambo huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Sao Hill, Godlisten Minja alisema kuwa maamuzi ya kufunga mtambo kwenye kiwanda hicho yamefanyika ili kuongeza ubora wa nguzo na kuongeza uzalishaji.
Amesema kuwa kwa kutumia mtambo huo nguzo zinakaushwa kati ya siku nne hadi 12 kutegemea hali ya ubichi tofauti na kutumia jua kukausha nguzo hizo ambapo nguzo hukaushwa kwa takriban miezi mitatu hadi minne.
Ameongeza kuwa mtambo huo una uwezo wa kukausha nguzo 800 hadi 900 kwa wakati mmoja kutegemeana na ukubwa wa nguzo.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameipongeza Sao Hill kwa kufunga mtambo huo wa kisasa ambao haukuwepo hapa nchini na kufanya upanuzi wa uzalishaji wa nguzo katika kiwanda hicho.
Amewahakikishia wazalishaji hao na wengine uhakika wa soko la nguzo hizo kwani kazi ya usambazaji umeme mijini na vijijini inaendelea. Aliwataka pia kuongeza uzalishaji wa nguzo hizo.
Amesema kuwa Serikali inategemea kuwa bei ya nguzo hizo zitapungua kutokana na kuongezeka kwa viwanda vya nguzo ambavyo kwa sasa ni zaidi ya 11 .
Aidha amesisitiza kuhusu ubora wa nguzo zinazozalishwa nchini na uhakika wa upatikanaji wa nguzo hizo ili kutokwamisha kazi ya usambazaji umeme.
Hata hivyo Waziri amelisisitiza Shirika la Umeme Tanzania na Wakala wa Nishati Vijijini kuhakikisha kuwa nguzo zinazotumika kwenye miradi ya umeme zinakuwa na ubora stahiki na wahakikishe malipo ya nguzo yanafanyika kwa wakati.
“Mahitaji ya nguzo kwa mwaka ni takriban milioni 4.5 wakat uzalishaji ni milioni 13 hivyo hakuna visingizio vya kutokuwepo kwa nguzo nchini” Amesema Kalemani.