Shirikisho la soka Barani Afrika ‘CAF’ limepanga wiki ijayo kuvitembelea viwanja vitakavyotumika kwenye michezo ya hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ili kuona uwezekano wa kuvifanyia majaribio ya teknolojia ya VAR.
Awali teknolojia hiyo ilikuwa ikitumika kwenye mchezo wa hatua ya Fainali tu, lakini kwa mwaka huu ‘CAF’ wataitumia kuanzia michezo ya Robo Fainali itakayoanza mwezi ujao.
Uwanja wa Benjamini Mkapa ni moja ya viwanja vitakavyotumika kwenye hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya mabingwa Afrika, kama uwanja wa nyumbani wa Simba SC.
Simba SC ilitinga hatua Robo Fainali kwa kuongoza msimamo wa ‘Kundi A’ kwa kufikisha alama 13, lililokua na timu za Al Ahly ya Misri iliyoshika nafasi ya pili kwa kuwa na alama 11, AS Vita Club ya DR Congo yenye alama 7 na Al Merikh ya Sudan inayoburuza mkia kwa kuwa na alama 2.