Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umepanga kufungua kesi mahakamani kupinga hatua ya jeshi la polisi kuzuia maandamano yao ya amani nchi nzima, yaliyolenga kupinga vitendo vya mauaji wilayani Kibiti mkoani Pwani.
Jeshi la Polisi lilizuia maandamano hayo hivi karibuni kwa sababu ambazo ilieleza kuwa yangeingilia oparesheni ya jeshi hilo ya kuwasaka wahusika wa mauaji ya polisi, viongozi na baadhi ya wananchi katika eneo hilo.
Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa jana aliviambia vyombo vya habari kuwa zuio hilo lililotolewa na jeshi la polisi halikuwa na sababu za msingi kisheria za kuweza kuzuia maandamano yao ya amani.
“Jeshi la polisi lina mamlaka kisheria ya kukataa kutoa ulinzi katika maandamano ya amani lakini sio kuyazuia,” alisema Olengurumwa kupitia taarifa ya mtandao huo kwa vyombo vya habari.
“Ni vyema kufahamu kuwa maandamano ya amani ni haki ya kikatiba hususan pale ambapo kuna vitendo vibaya vya mauaji ya askari polisi na raia,” anakaririwa na kuongeza kuwa mtandao huo unajipanga kwenda mahakamani.
Kwa mujibu wa Ole Ngurumwa, maandamano hayo ya amani ni muhimu kusaidia juhudi za kukomesha vitendo hivyo kwani mauaji yameendelea kuripotiwa wilayani Kibiti ingawa juhudi za kuyadhibiti zinaendelea kuchukuliwa.
Julai 6 mwaka huu, jeshi la polisi lilizuia maandamano hayo likieleza kuwa yangeweza kuingilia mbinu za kiintelijensia zinazoendelea katika kuwasaka wahusika wa mauaji hayo.
Tayari jeshi la polisi limeshawakamata watuhumiwa kadhaa na hivi karibuni lilifanikiwa kuwaua watu wanaosadikika kuwa ni majambazi mkoani Mwanza. Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi hilo, baada ya kuwapekuwa waliwakuta na silaha za moto pamoja na nguo za kuficha sura zao.