Mtangazaji maarufu wa radio nchini Uganda, Siima K K Sabiti anatarajia kufunga ndoa ‘feki’ na rafiki yake usiku huu, kwa lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya tendo jema.
Hatua hiyo imekuja kama sehemu za jitihada za kutafuta fedha za kumsaidia mwandishi Lulu Jemimah, kugharamia masomo yake ya shahada katika Chuo Kikuu Cha Oxford.
She ready! #TheKaBernzWedding pic.twitter.com/jAh1Is9a4Z
— Siima K K Sabiti (@kanyindo) October 26, 2018
Lulu (32) alishika vichwa vya habari hivi karibuni baada ya kuandaa ndoa yake peke yake bila mwenza (kujioa) ambapo alidai pamoja na mambo mengine alipanga kuchangisha fedha za kumuwezesha kusoma shahada chuo kikuu cha Oxford.
Mwanamke huyo alisema kuwa alichukua uamuzi huo baada ya kuona anapata msukumo mkubwa wa jamii kuhusu kufunga ndoa. Alisema anakumbuka akiwa na umri wa miaka 16 tu, baba yake aliandaa hotuba ambayo alidai anaitunza kwa ajili ya ndoa ya mwanaye.
Alisema hata wakati huu alipowaambia watu wake wa karibu kuwa amepata nafasi ya kwenda kusoma nje ya nchi, wao walijikita katika kumsukuma kufunga ndoa kwanza.
“Watu wengi walikuwa wananiambia, ‘unaenda nje ya nchi sasa, lakini utaenda kukutana na mwanaume wa aina gani? Kwanini usiolewe na mwanaume hapa ndipo usafiri?’” alisema Lulu.
Hali hiyo ilimfanya kuandaa harusi yake mwenyewe ambayo iligharimu $1.50 (Sh. 3,438) tu.
Lulu amepata wa kumuunga mkono katika kampeni yake, mtangazaji Sabiti amelenga kusaidia kusanya $12,000 kwa ajili yake kupitia harusi yake hiyo feki atakayofanya na rafiki yake wa kiume.
“Tunatumaini kuwa tutaleta utofauti. Tuko kwenye uchumi wa Uganda, Lulu anatakiwa kukusanya fedha za Uingereza (Pauni). Nina mtazamo chanya kuwa tunaweza kuchangia kiasi fulani kumsaidia kumaliza shahada yake,” Sabiti ambaye amefanya kazi kwa muda mrefu na X Fm aliiambia BBC.
“Kuna wasichana wengi wadogo ambao wanakumbwa na msukumo wa jamii kuhusu kuolewa. Wengi kama Lulu wameamua kujiendeleza kielimu zaidi, kwenye kazi zao au kuanzisha biashara kabla ya kuanza maisha ya ndoa,” aliongeza.
Sabiti amesema kuwa hatua ya kuepuka msukumo huo imeanza taratibu lakini wanaamini baada ya muda utakuwa utaratibu uliokubalika.