Mahakama ya Hakimu Mkazi Mombasa nchini Kenya imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela, Mtanzania aliyekutwa na hatia ya kusafirisha madawa ya kulevya aina ya Heroin.
Mtanzania huyo aliyetajwa kwa jina la Hussein Masoud Eid alihukumiwa kifungo hicho jana ambapo mbali na hukumu ya kifungo jela ametakiwa kulipa faini ya Sh. 90 milioni za Kenya. Endapo atashindwa kulipa kiasi hicho kama faini, atatakiwa kutumikia miaka mingine mitano jela.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa Mombasa, Edgar Kagoni alisema kuwa ingwa Eid alikiri kuhusika kusafirisha madawa ya kulevya na kueleza kuwa alikuwa anatumiwa na wenye mtandao huo, anampa adhabu kali ili iwe fundisho kwa jamii.
“Inaonekana mtuhumiwa hakuwa peke yake, alikuwa anapita njia, nitatoa adhabu kali sio tu kwa kumuadhibu kwa kukubali kutumika na wafanyabiashara wa dawa za kulevya bali pia kuzuia watu wengine wanaoweza kushawishika kusafirisha madawa hayo ya kulevya,” alisema Hakimu Kagoni.
Awali, mwendesha mashtaka aliiomba Mahakama kumfunga mtuhumiwa kifungo cha maisha ili iwe fundisho kwa jamii, lakini wakili wake aliomba apunguziwe adhabu kwani ameshakaa mahabusu kwa kipindi cha miaka mitatu.
Hata hivyo, maombi yote yaliishia kwenye nyundo ya miaka 30 jela na faini ya Sh.90 milioni za Kenya.