Mtanzania Gibson Kawago (24), ambaye ni miongoni mwa vijana 17 walioteuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa viongozi vijana wa kusongesha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs amesema atatutumia ugunduzi wake kuchakata betri chakavu za kompyuta, kutengeneza betri za kuzalisha umeme katika kulinda na kuhifadhi mazingira.
Gibson ameyasema hayo wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa jijini Dar es salaam, na kusema amepokea kwa furaha uteuzi huohuku akisema, “nina furaha kubwa sana kuweza kuteuliwa na Umoja wa Mataifa kwa kutambua mchango wangu kwenye kutatua matatizo katika jamii hii ninayotoka.”
Amesema, anaamini kilichomfanya ateuliwe kuwa balozi ni kazi yake ya kubuni mbinu za nishati salama, na kudai kuwa chanzo cha ubunifu huo ni kifo cha bibi yake akisema, “Kuna siku nikiwa kijijini nilikuwa natumia simu yangu kumuonesha bibi picha za harusi. Katikati betri ikaisha na hatukuwa na umeme na kesho yake nikasafiri umbali mrefu hadi mjini kupata betri.”
“Kwa hiyo wakati napata maumivu yale na kuwaza ni watu wangapi wanapata matatizo ya namna hiyo nilipofika Dar es salaam wakati nasoma Chuo Kikuu cha Teknolojia ya Ufundi, DIT nikaanza kutafiti ni kwa vipi naweza kutengeneza betri inayohifadhi umeme, hadi kufanikiwa jambo hili kama hatua za awali,” amesema Gibson.
Hata hivyo, Gibson ameongeza kuwa, kipindi cha miaka miwili cha nafasi hiyo ya kijana kiongozi wa kusongesha SDGS, atajitahidi kuwa balozi mzuri kuhakikisha vijana wenzake wanafahamu namna ya kutunza mazingira na kunajua ni jinsi gani watatafuta fursa tofauti za kutatua matatizo katika jamii zao na kutunza mazingira.