Inaelezwa kuwa Nahodha na Kiungo wa Coastal Union, Mtenje Albano anakaribia kumalizana na Dodoma Jiji kwa ajili ya kuitumikia msimu ujao wa Ligi Kuu.

Kiungo huyo mkabaji anakwenda kuongeza nguvu katika sehemu ya katikati ya uwanja akisaidiana na Rajabu Mgalula, Salmin Hoza na Enrick Nkosi.

Inadaiwa tayari kiungo huyo yupo jijini Dodoma kumalizana na walima Zabibu hao huku ikielezwa pia timu ya Ihefu inahitaji huduma yake kwa udi na uvumba.

Kiongozi mmoja anayeshughulikia masuala ya usajili katika klabu hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake amesema awali walimpelekea ofa kiungo huyo, lakini aliikataa na baada ya kuongeza dau alikubali.

“Kuna vita kubwa na Ihefu, ila tunaamini tutamsajili kwani ni chaguo la kocha Mellis Medo,” amesema kiongozi huyo.

Dodoma Jiji msimu uliopita ilianza na kocha Masoud Djuma kutoka Burundi na mambo yalipokwenda hovyo ilimleta Medo na kuiwezesha kumaliza katika nafasi ya tisa ikikusanya alama 37 kama ilizomaliza nazo Geita Gold na Tanzania Prisons.

Katika hatua nyingine inaelezwa kwamba uongozi wa klabu hiyo umemuongezea mkataba wa mwaka mmoja Medo kwa ajili ya kuitumikia msimu ujao.

Kocha huyo alijiunga na klabu hiyo Oktoba, mwaka jana kuchukua nafasi ya Djuma ambaye alitimuliwa kutokana na matokeo mabaya ya timu hiyo.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema uongozi umeridhika na kazi ya kocha huyo na kuamua kumuongeza mkataba huo.

Mvua, maporomoko vyaleta maafa 41 wakifariki
West Ham United wanaisubiri Arsenal