Joshua Lawrence kutoka Mkoani Mbeya amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwania Urais wa Tanzania kupitia chama cha ACT Wazalendo na kuahidi kuhakikisha kila mwananchi atafuga Kuku wasiopungua 1000.
Ametaja vipaombele vyake kuwa,ni kuwekeza katika kilimo cha mazao ya chakula na biashara, elimu ya ufugaji kuku, na kuhakikisha elimu ya bangi katika kuzalisha nyuzi za viwanda na chakula cha kurutubisha mifugo kama kuku.
“Nikizungumzia bangi si wawe wanavuta, bali ni kuwawezesha kujua madhara yake na faida wenzetu wanayoipata katika mataifa makubwa yenye virutubisho katika ulishaji wa chakula cha kuku na kuzalisha nyuzi za kutengenezea nguo kama ilivyo kwa zao la pamba” Amesema mgombea huyo.
Katibu wa ACT – Wazalendo mkoa wa Mbeya, Geofrey Sanga amesema tangu kuanza uchukuaji fomu, wamepata wagombea ubunge majimbo ya Mbeya, Rungwe, Mbarali na mmoja wa Urais.
Ikumbukwe kuwa hii itakuwa mara ya pili kwa ACT – Wazalendo kusimamisha mgombea Urais baada ya Anna Mghwira kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi wa mwaka 2015.