Wakati klabu mbalimbali zikianza maandalizi ya msimu ujao huko Mtibwa Sugar ikiwa kimya kutokana na ubize wa viongozi kuendelea na mchakato wa kumpata kocha mkuu atakayekinoa kikosi hicho.
Viongozi hao wamekuwa bize kupitia majina ya makocha waliotuma (CV) wasifu wao ili kuifundisha kwa msimu ujao lakini Mwanaspoti limedokezewa upepo mkubwa umeangukia kwa Kocha Habibu Kondo.
Katika majina yaliyokuwa yanapewa nafasi kwenye kiny’anganyiro hicho alikuwa ni Charlse Boniface Mkwasa ‘Master’, Juma Mwambusi na Malale Hamsini ambaye hata hivyo imekuwa ngumu kumtoa JKT Tanzania.
“Katika vikao vyetu Kondo amekuwa na nafasi kubwa sana ya kupewa timu ingawa bado uamuzi wa mwisho haujafikiwa ila leo (Jumatatu) tutafunga zoezi hili rasmi,” kimesema chanzo chetu.
Afisa Mtendaji Mkuu, Swabri Aboubakar amesema suala la wao kuchelewa kutangaza kocha ni kutokana na kutaka kujiridhisha na kufanya uamuzi usahihi.
Kwa upande wa Kondo akizungumza kuhusu jambo hilo alisema bado hajajua hatima yake msimu ujao ingawa kama itatokea timu yoyote na kuweka ofa mezani basi atazungumza nayo.
Mbali na Kondo, Kocha Msaidizi wa Ihefu FC Zubery Katwila naye pia anapigiwa chapuo.
Mtibwa ilioanza msimu vibaya na kunusurika kushuka daraja, haina kocha mkuu tangu alipoondoka Salum Mayanga iko chini ya msaidizi, Awadh Juma ‘Maniche’.