Kikosi cha Mtibwa Sugar huenda kikarudi kwenye Uwanja Manungu mwezi huu Desemba 2021, kufuatia maboresho ya uwanja huo kukamilika kwa asilimi 80.
Uwanja huo ambao ndio nyumbani kwa Mtibwa Sugar ulifungiwa na Bodi ya Ligi ‘TPLB’ kufuatia kukosa vigezo vya kutumiwa katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Mtibwa Sugar Thobias Kifaru amesema kwa sasa uwanja wao umefikia asilimia 80 ya maboresho, hivyo wanatarajia kuona kikosi chao kikirejea uwanjani hapo.
Amesema Uongozi unapambana kukamilisha maboresho hayo kwa asilimi 100, ili kuishawishi ‘TPLB’ kuwapa ruhusa ya kuutumia kwa michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.
“Uwanja wa Manungu upo katika hatua za mwisho, tunaamini maboresho yanayofanywa hapa yatafanikisha kikosi chetu kurejea na kucheza hapa katika michezo yetu ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.”
“Kwa sasa maboresho yamefikia asilimia kama 80, tunaamini asilimia 20 zilizobaki zitakamilika muda mfupi ujao na huenda kikosi chetu kikacheza mchezo ujao wa Ligi Kuu katika uwanja huu ambao tulikua tumeuzoea.” Amesema Kifaru.
Baada ya Uwnaja wa Manungu kufungiwa, Mtibwa Sugar ilihamia mjini Gairo kwenye Uwanja wa CCM Gairo, kabla ya kuhamishia mawindo yao katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.