Timu ya soka ya Mtibwa Sugar usiku wa leo itashuka dimbani kuwania Kombe la Mapinduzi dhidi ya URA ya Uganda kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Mtibwa Sugar imeingia Fainali baada ya kuwatoa waliokuwa mabingwa watetezi, Simba SC Jumapili kwa kuwafunga bao 1-0.

URA nayo imetinga fainali, baada ya kuwatoa mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga SC kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.

Hii itakuwa mara ya tano kwa Mtibwa Sugar kufika fainali, baada ya awali kucheza fainali nne na kutwaa taji mara moja, 2010 ilipoifunga Ocean View ya Zanzibar.

Mtibwa iliingia fainali mwaka 2007 na kufungwa na Yanga SC – wakati 2008 na 2015 ilifungwa na Simba SC mara zote.

URA ambao wanacheza mashindano haya kwa mara ya pili, hawajawahi kufika fainali, lakini mwaka 2014 taji la Mapinduzi lilipanda ndege kwenda Uganda, lilipochukuliwa na KCCA walioifunga Simba SC katika fainali.

Mchezo huu pia unatazamwa kama sehemu ya watanzania kuhitaji kulipiza kisasi cha kufungwa na Uganda katika mchezo wa kusaka nafasi ya kucheza fainali za mataifa bingwa barani Afrika CHAN (2015), katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Aman visiwani Zanzibar kwa kukubali kichapo cha mabao matatu kwa sifuri.

Nisher azungumzia Mpango wa Kuokoka, ajibu tuhuma za kutumia fedha za baba kuchapia
Saad Kawemba: Bado Tutaendelea Kuutumia Uwanja Wetu CAF