Kocha Msaidizi wa Singida Fountain Gate FC, Thambo Senong amesema mechi yao iliyopita dhidi ya Mtibwa Sugar imewapa kipimo kizuri kuelekea mchezo wao wa kesho Jumapili (Oktoba 08) dhidi ya Simba SC.
Singida FG juzi Alhamis (Oktoba 05) ilipata ushindi wa kwanza tangu pazia la ligi hiyo kufunguliwa baada ya kuifunga Mtibwa Sugar bao 1-0, uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
Katika michezo minne iliyocheza Singida FG imeshinda mchezo mmoja, imetoa sare mbili na imepoteza mchezo mmoja ikikusanya alama tano na inashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi kuu Tanzania Bara.
Akizungumza mjini Singida, Thambo amesema mechi na Mtibwa Sugar walicheza vizuri na wametumia mchezo huo huo kujiandaa na mchezo wao wa kesho Jumapili (Oktoba 08) dhidi ya Simba SC.
Amesema wameridhishwa na kiwango cha wachezaji walichokionyesha kwenye mchezo uliopita na anaamini wataendeleza kile walichokifanya kwenye mchezo wa kesho.
“Tunasahau matokeo ya mechi iliyopita dhidi ya Mtibwa, tunaangalia mbele sasa, mchezo wetu ujao ni dhidi ya Simba SC nyumbani, tunahitaji kupata matokeo chanya kulingana na ubora wa wapinzani wetu,” amesema Thambo
Ameongeza wamefanyia kazi mapungufu madogo waliyoyaona kwenye mchezo wao dhidi ya Mtibwa Sugar ikiwemo umakini wa wachezaji wake hasa safu ya ushambuliaji kutumia nafasi zinazopatikana kupata matokeo mazuri.
“Haitakuwa mechi rahisi, tunaenda kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu kuhakikisha hatufanyi makosa ambayo yatatuadhibu kwa kupoteza nyumbani, Simba ni timu kubwa na ina wachezaji wazuri hivyo lazima tujipange vizuri kuwakabili ” amesema Kocha huyo msaidizi.