Madaktari wa magonjwa ya sikio, pua na koo (E.N.T) katika Hospitali ya Benjamini Mkapa jijini Dodoma wamefanikiwa kumfanyia upasuaji mtoto wa miaka 14 na kuondoa jiwe lililonasa ndani ya tundu la pua yake ya upande wa kulia kwa miaka 12.
Kwa mujibu wa Daktari bingwa, Faustine Bakanu, mtoto huyo alipelekwa hospitalini hapo baada ya wazazi wake kuzunguka katika hospitali kadhaa bila mafanikio.
Amesema baada ya kumfanyia uchunguzi walibaini kuwepo kwa jiwe hilo ambalo walilitoa baada ya kumfanyia upasuaji na kwasasa mtoto huyo anaendelea vizuri na ameruhusiwa kurejea nyumbani.
Mama mzazi wa mtoto huyo mkazi wa Tanga, ameeleza kuwa wanahisi jiwe liliingia puani kwa mtoto wake wakati wa michezo ya watoto.
Ameishukuru hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kumtibu mtoto wake ambaye amehangaika naye toka akiwa na umri wa miaka miwili mpaka sasa anaumri wa miaka 14.
Amesema hali ya mtoto wake ilikuwa mbaya kwani alikuwa ameanza kutoa harufu mbaya puani na kufuatwa na nzi.
” Shida ya mtoto wangu ilianza toka akiwa na miaka miwili, nimehangaika naye sana, nimeenda hospitali mbalimbali bila mafanikio mpaka nduguyangu mmoja aliponishauri nifike hapa kujaribu kupata matibabu”
” Kwakweli namshukuru Mungu sasa hivi mwanangu anaendelea vizuri sana, hakuna harufu wala nzi” Ameeleza mama huyo kwa furaha.