Kijana Hamimu Mustapha Baranyikwa (15), mkazi wa kijiji cha Nyakanazi, Biharamulo, Mkoani Kagera, amesimulia jinsi alivyougua maradhi ya ngozi mwilini mwake kwa muda mrefu kabla ya kupata msaada asioutarajia kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan wakati alipofanya ziara mkoani humo tarehe 16 Oktoba, 2022.
Mara kwa mara Rais Samia anapokuwa ziarani sehemu mbali mbali hapa Tanzania hukutana na watu wakamwelezea shida zao binafasi na akazipatia ufumbuzi.
Lakini tukio moja la Oktoba 2022 lilikuwa la aina yake na limebadili maisha ya mtoto mmoja.
Katika msafara wake akiwa ziarani mkoani Kagera, Rais Samia alimkuta mtoto wa kiume Hamimu Baranyikwa akiwa amekaa pembezoni mwa barabara akionekana kuwa na huzuni kubwa.
Ngozi ya mtoto huyu mwili mzima ilikuwa imeharibika vibaya kwa maradhi.
“Watu walikua wananiogopa, nilikua sichezi na watoto wenzangu. Hata watu wazima walikua wakiniona tu wananikimbia,” alisema Hamimu.
“Niliteseka kwa waganga, hadi nikasema mniache tu nife. Nilikosa amani, nikawa nakaa tu ndani. Sitoki nje.”
Baada ya kupata maelezo yake, Rais aliagiza mtoto huyo apelekwe Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam kufanyiwa uchunguzi.
Habari njema ni kwamba, takriban miezi sita tangu Hamimu aanze kutibiwa, amepata nafuu ya hali ya juu.
Hamimu sasa ameruhusiwa kutoka hospitalini kwenda nyumbani Aprili 19, 2023.
“Sasa naweza kushika vitu na mkono na hata kula ugali na sura yangu inaonekana,” alisema Hamimu akiwa hospitali ya Muhimbili baada ya matibabu.
Hamimu alipokelewa na kuanza kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tarehe 21 Oktoba, 2022 kwa msaada wa Rais Samia.
Na sasa ameruhusuiwa kurejea nyumbani kwa wazazi wake Nyakanazi Mkoani Kagera baada ya hali yake kuimarika na amemshukuru Rais Samia kwa moyo wake wa kumsaidia na kuokoa maisha yake.
“Tumehangaika hapa na pale hadi imeshindikana yeye akaniona. Huku kwetu kuna watu wenye hela lakini wameshindwa kunisaidia,” alisema.
“Namshukuru Mama Samia. Ingekuwa inawezekana, nilikua natamani nimuone hivi kwa macho kwa jinsi alivyonisaidia.”