Wafanyakazi wa uwanja wa ndege nchini Mauritius wamempata mtoto mchanga mvulana aliyetelekezwa kwenye choo cha kuhifadhia taka katika choo cha ndege.
Kutokana na tukio hilo, wanamke mwenye umri wa miaka 20 kutoka Madagascar, anayeshukiwa kujifungua kwenye ndege, alikamatwa.
Ndege ya Air Mauritius, iliyowasili kutoka Madagascar, ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sir Seewoosagur Ramgoolam tarehe 1 Januari. Limeandika shirika la BBC
Maafisa wa uwanja wa ndege walifanya ugunduzi huo walipoikagua ndege hiyo kwa ukaguzi wa kawaida wa forodha na walimkimbiza mtoto huyo katika hospitali ya umma kwa matibabu.
Mwanamke anayeshukiwa kuwa mama wa mtoto huyo ambaye awali alikana mtoto huyo kuwa ni wake, alifanyiwa uchunguzi wa kimatibabu ambao ulithibitisha kuwa alikuwa amejifungua.
Hata hivyo aliwekwa chini ya uangalizi wa polisi katika hospitali hiyo na inasemekana kwamba yeye na mtoto wanaendelea vizuri.
Mwanamke huyo wa Madagascar, ambaye alifika Mauritius kwa kibali cha kufanya kazi cha miaka miwili, atahojiwa baada ya kuachiliwa kutoka hospitalini na kushtakiwa kwa kumtelekeza mtoto mchanga.