Saif Al Islam Gaddafi, mtoto wa kiume wa Rais wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi ana sifa za kugombea nafasi ya urais wa nchi hiyo utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Spika wa Bunge la Libya, Aguila Saleh Issa amewaambia waandishi wa habari kuwa kutokana na mabadiliko ya sharia, Saif anaweza kugombea nafasi hiyo kama ilivyo kwa raia yeyote wa nchi hiyo aliye huru.
“Tumeanza kutumia sharia mpya ambayo inaondoa utengano katika siasa. Sasa hivi kila raia wa Libya, ambaye hatumikii kifungo chochote chini ya sharia, anayo haki ya kugombea urais kuona kama wananchi wengi zaidi wanamhitaji,” alisema.
Msemaji wa familia ya Gaddafi alieleza mwaka jana mwishoni kuwa Saif ana idadi kubwa ya watu wanaomuunga mkono na kwamba ndiye mwenye uwezo wa kurejesha utulivu nchini humo tangu baba yake alipoondolewa madarakani na kuuawa mwaka 2011.
Tangu Gaddafi alipoondolewa madarakani na kuuawa kufuatia vita iliyoendeshwa na jeshi la waasi walioungwa mkono na mataifa ya Magharibi, Libya imekuwa katika machafuko.