Mtoto mwenye umri wa miezi nane ameripotiwa kuwa katika hali mbaya akipatiwa matibabu hospitalini baada ya kubakwa na mtu aliyetambulika kuwa ni binamu yake jijini Delhi nchini India.
Jeshi la polisi limeeleza kuwa tukio hilo lilitokea Jumamosi iliyopita ambapo wanamshikilia kijana mwenye umri wa miaka 28 aliyekuwa akifanya kazi za vibarua.
Mkuu wa Tume ya Wanawake ya Delhi, Swati Maliwal ambaye alimtembelea mtoto huyo hospitalini amesema mtoto yuko katika hali mbaya na kwamba madaktari wamepanga kumfanyia upasuaji kwa saa tatu.
Aidha, Maliwal aliweka kwenye akaunti yake ya Twitter maelezo yanayoonesha jinsi ambavyo jiji hilo limehuzunishwa na kitendo hicho cha kikatili na kuuliza umma nini hasa kinapaswa kufanyika.
“Tufanye nini? Ni kwa namna gani Delhi inaweza kulala leo wakati mtoto wa miezi 8 amebakwa vibaya katika jiji hili? Je, tumekosa kuwa na hisia za utu au tumeamua kuwa hii ndiyo hatma yetu,” inaeleza tweet ya Maliwal.
- Kenyatta: Ole wake atakayerusha mubashara kuapishwa kwa Odinga
- Video: Mizinga ya nyuki yanaswa kwenye uwanja wa ‘kumuapisha’ Raila
Alimtaka Waziri Mkuu, Narendra Modi kuhakikisha kuwa jeshi la polisi na jamii vinaimarishwa katika kuwalinda watoto pamoja na kuweka sheria kali zaidi.
Vitendo vya unyanyasaji wa kingono nchini India vimeongezeka tangu mwaka 2012 baada ya kundi la wanaume kuvamia basi, kumbaka na kisha kumuua kikatili mwanafunzi wa kike mwenye umri wa miaka 23.