Jeshi la Polisi mkoani Iringa linafanya Uchunguzi dhidi ya watuhumiwa wa wizi wa fedha za kitanzania kiasi cha Sh 2,129,856,000/= mali ya Kampuni ya SELCOM PAYTECH LIMITED.
Imeelezwa kuwa Wakala wa Selcom aitwaye Tyson Kasisi wa mkoani Iringa kupitia huduma ya ‘Selcom Pay’ isivyo halali alihamisha fedha kwenda nambari mbalimbali za simu na kisha kuchukuliwa taslimu kupitia wakala wa huduma za kifedha za mitandao mbalimbali ya simu pamoja na akaunti za Benki.
Wizi wa fedha hizo ulifanyika kwa njia ya mtandao katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Iringa, Dar es Salaam na Morogoro kati ya Novemba 9 hadi 27, 2021 baada ya wakala huyo Tyson Kasisi kufanikiwa kuchezea mfumo wa kieletroniki wa ‘Selcom Pay’ unaomilikiwa na Kampuni ya SELCOM PAYTECH LTD.
Wakala huyo kwa njia ya udanganyifu alianza kujitumia fedha pamoja na kuwatumia watu wengine na kwa kushirikiana na genge lake la uhalifu walifanikiwa kuiba kiasi hicho cha Shilingi za kitanzania 2,129,856,000/=
Jeshi hilo limefanikiwa kukamata (Kuokoa) fedha taslimu Sh 956,974,000 kutoka kwa watuhumiwa na washiriki wa uhalifu huo ambao walipokea sehemu ya fedha hizo kwa ajili ya kuzificha katika maeneo mbalimbali ikiwemo makazi na shambani.
Aidha, kiasi cha fedha za kitanzania Sh 121, 215,783 zimezuiliwa katika moja ya benki za biashara mkoani Iringa ikiwa ni mazalia ya uhalifu.
Upelelezi uliofanyika mpaka sasa umebaini kuwa genge la uhalifu na wizi wa fedha za Selcom uliongozwa na watu watatu ambao ni Tyson Kasisi, Patrick Chalamila na Evaristo Chalamila ambao wamebainika kuwa wanufaika wakuu wa uhalifu huo.