Jeshi la polisi nchini Kenya limeripoti taarifa ya ‘mtuhumiwa mbabe’, aliyekuwa anakimbizwa hospitalini baada ya kujeruhiwa na kundi la watu wenye hasira kali, lakini alikata pingu na kutoroka akiwa njiani.
Imeelezwa kuwa usiku wa kuamkia Ijumaa, mtuhumiwa aliyetajwa kwa jina la Francis Mwangi alikuwa akipelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu akisindikizwa na askari sita waliokuwa kwenye magari mawili.
Polisi wameeleza kuwa Mwangi alishambuliwa na wananchi wenye hasira kali baada ya kutuhumiwa kumuua rafiki wake wa kike katika eneo la Kirima, Alhamisi wiki hii.
Mtuhumiwa huyo alikuwa kwenye gari moja aina ya Land Cruiser, ndani yake kukiwa na askari watatu. Nyuma ya gari hilo kulikuwa na gari lingine binafsi likiwa na askari wengine watatu waliohakikisha usalama kwa mbali. Lakini kwa kujiridhisha zaidi, mtuhumiwa huyo alikuwa amefungwa pingu muda wote.
Kwa mujibu wa ripoti ya Polisi, ambayo imeripotiwa pia na Citizen TV ya Kenya, wakiwa njiani, mtuhumiwa alianzisha vurugu kubwa akipambana na maafisa waliokuwa kwenye gari la polisi. Kutokana na hali hiyo, dereva alisimamisha gari.
“Dereva aliposikia vurugu alisimamisha gari ili kufahamu kilichokuwa kinaendelea. Mtuhumiwa alifanikiwa kukata pingu, akawazidi nguvu askari hao na kukimbilia vichakani kabla gari lenye polisi waliokuwa wanafuata nyuma kuwasili,” ripoti ya polisi imeeleza.
Maafisa wa polisi waliomba msaada wa mbwa maalum kumsaka mtuhumiwa huyo. Hata hivyo, hadi kufikia Ijumaa asubuhi mbwa wa polisi pia hawakufanikiwa.
Wakati msako wa polisi ukiendelea, wananchi wenye hasira kali walivamia nyumba ya mtuhumiwa na kuichoma moto, Ijumaa asubuhi.
Hata hivyo, kwa kuwa dunia imekuwa kama mtaa, sehemu za kujificha zinaendelea kuwa adhimu. Wananchi walifanikiwa kutambua eneo la maficho ya mtuhumiwa huyo, wakamkamata katika eneo la Emboita na kuanza kumshushia ‘kipigo cha mbwa koko’.
Filamu hiyo ya kweli ilikamilika baada ya polisi kupewa taarifa na kufika haraka katika eneo la tukio, wakamkamata tena mtuhumiwa huyo mbabe. Sasa anashikiliwa katika kituo cha polisi cha Nakuru.
Video zilizosambaa zinaonesha umati wa watu wakiwa wamekusanyika katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Nakukuru. Wananchi hao wanataka polisi wawakabidhi mtuhumiwa huyo ‘wamalizane naye’.