Muasisi wa jina ‘Bongo Flava’ ambaye ni miongoni mwa watangazaji wa kwanza wa redio za FM nchini Tanzania, Mike Mhagama, amekuja na kipindi (podcast) kiitwacho ‘Maktaba ya Bongo Flava’, ambacho atakitumia kuelezea historia ya muziki huo.

Mike amesema kuwa kipindi hicho kitakuwa katika mfumo wa makala ambayo itajikita katika kuzungumzia muziki huo kwa kumulika historia yake, kutafakari ulipo sasa na maono ya unapoelekea.

“Pia, kutakuwa na majadiliano ya nini kifanyike zaidi kupanua wigo wake wa washabiki na biashara duniani,” amesema Mhagama na kuongeza, “msukumo wa kuandaa kipindi hiki ulitokana na maombi ya mashabiki wenyewe kuomba kuwepo na makala maalum kama haya hasa kwa vijana ambao hawafahamu historia halisi.”

Mwanahabari huyo ameongeza kuwa anataka kuweka ‘facts’ sawa kwani kumekuwa na upotoshwaji mkubwa wa makusudi kuhusu historia ya muziki wa Bongo Flava.

“Mwisho ni ushawishi wa rafiki yangu Fredrick Bundala ambaye alinisihi kushare ninachokifahamu kuhusu muziki huu ili wengi wapate kunufaika na kumbukumbu za muziki wa kizazi kipya. Natumaini wengi watafurahi na kuelimisha pia,” alisema.

Kipindi hicho kitakuwa kikitoka kila wiki siku ya Alhamisi kupitia jukwaa la kwanza Afrika la radio za kuweka vipindi mtandaoni (podcast), Afripods. Unaweza kusikiliza kipindi hicho kwa kuclick hapa > http://bit.ly/2h4ta2K . Unaweza kusikiliza kipindi hicho kwa kudownload app ya Afripods kwenye App store na Google Playstore.

Mahakama yamuachia Tundu Lissu kwa dhamana
Gambo amnyooshea kidole Lema, amtahadharisha