Mwanachama na Shabiki wa Simba SC Said Muchachu amesema bado anaamini klabu yake ina nafasi kubwa ya kutetea Ubingwa msimu huu 2021/22, licha ya kuachwa kwa alama 08 na watani zao Young Africans.
Simba SC ilifufua tena matumaini ya mbio za ubingwa baada ya kuibamiza Kagera Sugar mabao 2-0 juzi Jumatano (Mei 11), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dara es salaam, huku Young African ikishindwa kufurukuta kwenye micheza mitatu mfululizo kwa kuambulia matokeo ya sare ya bila kufungana.
Muchachu amesema bado ni mapema mno kukubali kuwa Simba SC imeshindwa kutetea taji lake msimu huu, kwa kigezo cha kuachwa kwa alama nyingi dhidi ya Young Africans.
Amesema Ligi bado inaendelea na lolote linaweza kutokea, hivyo yeye kama Shabiki na Mwanachama wa Simba SC hana shaka na suala la Ubingwa.
“Sisi ndio mabingwa watetezi, tunautetea ubingwa wetu kwa mwaka wa tano sasa, hatuwezi kukubali kuuchia ubingwa wetu kirahisi kihivyo, tunawambia wenzatu kuwa sisi ni Simba na letu ni moja, hivyo ni mapema sana kusema tumekubali kushindwa.”
“Mpaka sasa zimebaki alama 08, ninamwambia kabisa Mtani akipepesuka kidogo tu, Simba SC tunaendelea kutawala soka la Tanzania kwa kutwaa ubingwa wa tano mfululizo.”
“Tunajua Mtani ana Presha, kwa sabababu tunaendelea kumsogelea, wao walicheza michezo yao katika Ligi wakiamini kila kitu kitakuwa rahisi, sasa wamekutana na timu ambazo zinapambana ili zisishuke Daraja, kwa hiyo lazima mambo yawe magumu.”
“Mtani anakwenda Dodoma na akirudi atakwenda Mbeya, sasa ninamwambia kabisa mtani akianguka tu, sisi tutachukua tena ubingwa na ninasema kwamba kama watashindwa kuchukua ubingwa msimu huu basi hawatachukua baada ya miaka kumi.” amesema Muchacho
Young Africans itachza dhidi ya Dodoma Jiji FC Jumapili (Mei 15) Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma, huku Simba SC ikitarajia kucheza dhidi ya Azam FC Jumatano (Mei 18) Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es salaam.