Mastaa wawili wa Young Africans na Azam FC watarajie rungu la Sh 500,000 na kufungiwa mechi tatu kutoka bodi ya ligi kutokana na kitendo walichokifanya kwenye mchezo wa juzi, Jumatatu (Oktoba 23) uliomalizika kwa mwenyeji kuibuka na ushindi, huku presha kubwa ikiwa kwa Young Africans ambao wanaweza kumkosa kiungo wao kwenye mechi dhidi ya Simba SC.
Kwa mujibu wa kanuni ya 41:5 (5.4), kufanya kitendo chochote cha aibu, kama vile kukojoa uwanjani, kukataa kupeana mkono na mgeni rasmi, waamuzi na wachezaji wa timu pinzani, kutoa au kuonyesha ishara inayoashiria matusi ni kosa.
Feisal Salum wa (Azam FC) na Mudathir Yahya wa (Young Africans) wamezua taharuki kwa kutegeana kuingia eneo la kuchezea la Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Tukio hilo lilitokea wakati vikosi vya timu hizo vikiingia uwanjani hapo tayari kuanza dakika 45 za kipindi cha kwanza na wachezaji hao walisimama kwenye mstari wa kuingia eneo la kuchezea.
Fei Toto alikuwa anafanya mazoezi ya viungo kwa kunyoosha miguu huku Mudathir akikung’uta viatu vyake ili kuvuta muda wa nani awahi kuingia uwanjani kitendo ambacho bodi ya ligi inatafsiri kama imani za kishirikiana na kutoza faini.
Mastaa hao walikuwa nje kwa muda wakati wachezaji wenzao wakijipanga na kusalimiana, Feisal na Mudathir waliendelea kutegeana hadi zoezi hilo lilipokamilika huku kila kikosi kikienda upande wake.
Wakati taharuki kwa mashabiki ikiwa kubwa baada ya kushtukia kitendo hicho, ndipo Mudathir alipoamua kuwa wa kwanza kwenda kuungana na wenzake huku Feisal naye akifuata na kupiga picha za vikosi.
Msimu uliopita mastaa wa Simba SC na Young Africans Aziz Ki na Clatous Chama, walilipishwa faini ya Sh 500,000 na kufungiwa kutokucheza mechi tatu za Ligi Kuu Bara zilizokuwa zinafuata kwa kosa kama hilo.
Ilielezwa katika mechi namba 64 ambayo ilizikutanisha Young Africans na Simba SC katika Dimba la Mkapa Oktoba 23, 2022 walikwepa kusalimiana.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, adhabu hiyo ni kwa uzingativu wa kanuni ya 41:5 (5.4) ya ligi kuu udhibiti kwa wachezaji msimu uliopita.
Hii ina maana kama kamati itakaa mapema Fei na Mudathir wanaweza kukosa michezo mitatu ijayo, Young Africans mechi zao ni dhidi ya Singida, Simba SC na Coastal Union, huku Azam wakiwa wanasubiri kucheza na Namungo FC, Mashujaa FC na Ihefu FC.