Katika kuhakikisha bonde la Mto Ruaha Mkuu lililopo Iringa linalindwa, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi imeagizwa kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kutenga maeneo ya kilimo kuepukana na uharibifu wa mazingira katika vyanzo vya maji vya bonde hilo.
Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Kikosi kazi cha Taifa cha kunusuru na kuweka mikakati endelevu ya kulinda ikolojia ya Mto Ruaha Mkuu, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Richard Muyungi.
Amesema kuwa mpango kazi wa utoaji wa elimu kwa wananchi katika hali endelevu kwa vijiji 121 utasaidia kuwapatia elimu ya kutosha wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira ya Mto Ruaha Mkuu na vyanzo vyake.
Aidha, baadhi ya Wajumbe wa Kamati hiyo wamesisitiza juu ya Watendaji wa Wilaya hiyo kuwa makini katika utendaji wao wa kazi na kuhakikisha kuwa wanasimamia sheria za ardhi na Mazingira ili kuwezesha ikolojia ya Mto Ruaha Mkuu inatunzwa vizuri.
Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamhuri William amekishukuru kikosi kazi hicho kwa kufika katika Wilaya yake na ameahidi kusimamia na kuyafanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na kikosi kazi hicho.
Hata hivyo, Kikosi kazi hicho kimeundwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ikiwa ni jitahada za kuweza kuokoa ikolojia ya Mto Ruaha Mkuu ambao unazidi kuharibika siku hadi siku kutokana na uharibifu wa vyanzo vya maji.