Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe bado anashikilia funguo za makazi rasmi ya rais wa nchi hiyo ikiwa ni miezi minne tangu alipolazimika kujiuzulu.
Taarifa hiyo imetolewa na aliyekuwa msemaji wake, George Charamba ambaye hivi sasa ni msemaji wa rais Emmerson Mnangagwa alipofanya mahojiano na gazeti la Standard.
“Kuna mtu haliambii taifa kuwa rais wa zamani bado anashikilia funguo za makazi rasmi ya rais,” alisema Charamba.
Aliongeza kuwa ingawa Mnangagwa hajahamia katika makazi hayo tangu alipoingia madarakani, ni jambo la kushangaza kuona bado funguo hazijarejeshwa wakati wakifahamu kuwa kuna mtu anapaswa kuingia.
Wiki iliyopita, gazeti la Daily News liliripoti kuwa Mugabe na mkewe bado hawajatoa vitu vyao ikiwa ni pamoja na samani binafsi ndani ya Ikulu ya nchi hiyo.