Familia ya Rais wa kwanza wa Zimbabwe, Robert Mugabe inadaiwa kuahidi kumpa kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC), Nelson Chamisa kiasi cha $24 milioni pamoja na magari 12 kusaidia kampeni zake.
Zimbabwe iko katika kipindi cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu ambapo Rais Emmerson Mnangagwa anagombea kupitia chama cha ZANU-PF alichokiasisi Mugabe.
Gazeti la Zimbabwe la Daily News limeeleza kuwa msaada huo kutoka kwa familia ya Mugabe unakuja kwa MDC kwa sharti kwamba itatenga viti 80 vya ubunge na nafasi ya Makamu wa Rais kwa ajili ya wafuasi wa chama ambacho kinaushirika na familia ya Mugabe.
MDC iko katika wakati mgumu kifedha ambapo hivi karibuni chama hicho kilianzisha kampeni ya kukusanya michango kutoka kwa wafuasi wake, kampeni ambayo imepewa jina la ‘Changia Mabadiliko’.
Mke wa Rais Mugabe, Mama Grace wanahusishwa na kukiunga mkono chama cha upinzani kipya cha National Patriotic Front.
Hata hivyo, gazeti hilo limeeleza kuwa masharti ya msaada huo kutoka kwa familia ya Mugabe yamepingwa vikali na baadhi ya viongozi waandamizi wanaomuunga mkono Chamisa kupitia MDC na muungano wake.