Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe ameuvuruga unabii wa wahubiri maarufu barani Afrika waliomtabiria kuwa hataweza kuuvuka mwaka 2015 baada ya kiongozi huyo kuupokea kwa furaha mwaka mpya 2016.

Januari 2015, mwanzilishi na kiongozi mkuu wa huduma ya kiroho wa BSI Winning Life Ministry ambaye ni mhubiri maarufu nchini Malawi, Austin Liabunya aliwaeleza waumini wake kuwa maisha ya rais Mugabe hayataweza kuuvuka mwaka 2015 huku akimtaka atubu vinginevyo ataenda kuzimu.

Miezi michache baadaye, mhubiri mwingine maarufu wa Malawi anayefahamika kama Kenneth Eagle wa kanisa la Holly Tabernacle  alieleza kuwa amepata maono kuwa Zimbabwe iko katika majonzi kutokana na kifo cha kiongozi wake mkuu.

“Zimbabwe haiko mbali kabla haijashusha bendera yake kwa siku kadhaa.. kama ishara ya heshima kwa kiongozi wao mpendwa,” alisema Eagle.

Utabiri huo umeonekana kuwavuruga watumishi hao wa Mungu kwakuwa baadhi ya waumini wao wameanza kuonesha shaka kutokana na ukweli wa utabiri wao katika mambo mbalimbali.

Februari 20 mwaka huu, Robert Mugabe atakuwa anatimiza umri wa miaka 92 na kuendelea kuwa rais mwenye umri mkubwa zaidi duniani akiitawala Zimbabwe tangu ilipopata uhuru wake Aprili 18 mwaka 1980.

Tayari chama chake cha ZANU kimempitisha kuwa mgombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2018 ambapo atakuwa na umri wa miaka 94 na endapo atafanikiwa atamaliza muhula wake akiwa ana umri wa miaka 99.

Samia Suhulu Atua Mgodini, Awaacha na 'neno'
Polisi amuua rafiki yake aliyemtembelea nyumbani