Mshambuliaji kutoka DR Congo Mugalu Chris Mutshimba Koppe Mugalu, ameshindwa kujizuia na kuanika wazi maisha anayopitia ndani ya kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC.
Mugalu alimaliza msimu uliopita na mabao 15 akishika nafasi ya pili ya wafungaji bora nyuma ya John Bocco, lakini msimu huu Mshambuliaji huyo mambo yamekuwa magumu kwake.
Amesema katika maisha yake ya soka la ushindani hajawahi kupitia kipindi kigumu kama wakati huu, ambapo anahaha kurejesha makali yake kama ilivyokua msimu uliopita.
“Kuna wakati huwa nashindwa kufunga, ila haijawahi kuwa kipindi kirefu kama hiki nilichonacho Simba SC, kwani mara nyingi hata nikitoka majeruhi nikirudi naendelea na ukali wangu wa kufunga mabao,” amesema Mugalu.
Mshambuliaji huyo amesema kwa sasa analichukulia changamoto anayopotia kama darasa la kujifua zaidi ili arejeshe makali yake binafsi kwa faida ya timu ya Simba SC.
“Binafsi naimani kubwa mno huu ni mwisho kwangu kucheza mechi nyingi bila kufunga nimefanya mazoezi yangu binafsi pamoja na kujiandaa vya kutosha kusikiliza yale ya benchi la ufundi ili kwenda kutimiza yale ambayo kila mmoja anatamani kuona kutoka kwangu,” amesema mchezaji huyo.
Jana Jumapili (Januari 30) Mugalu aliifungia Simba SC bao lake la kwanza msimu huu katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Dar City FC katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.