Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Chriss Mushimba Koppe Mugalu, ana matarajio ya kuwa sehemu ya kikosi cha mabingwa hao, kitakachoikabili Young Africans mwishoni mwa juma hili (Julai 03), Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Simba SC itakuwa wenyeji wa Young Africans, kwenye mchezo huo ambao ulisogezwa mbele, baada ya ule ya awali (Mei 08) kuahirishwa kwa sababu ambazo zilikua nje ya uwezo wa Shirikisho la soka nchini TFF pamoja na Bodi ya Ligi (TPLB).
Mshambuliaji huyo ambaye alikosekena kwenye mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Azam FC, uliochezwa mjini Songea mkoani Ruvuma mwishoni mwa juma lililopita, amesema anaendelea vizuri.
“Nilipata tiba nzuri kutoka kwa madaktari na yalikuwa maumivu pamoja na mshtuko baada ya kuchezewa rafu ya nguvu, lakini kwa sasa maendeleo yangu ni mzuri tofauti na awali,” amesema mshambuliaji kutoka DR Congo na kuongezea
“Ambacho nasubiria hapa ni kuungana na wachezaji wenzangu kwa ajili ya maandalizi ya mchezo unaofuata lakini kimaendeleo sasa nipo fiti.”
Tayari kikosi cha Simba SC kimesharejea jijini Dar es salaam, kuanza maandalizi ya mchezo ujao dhidi ya Young Africans, kikitokea mjini Songea mkoani Ruvuma, kilipoichapa Azam FC bao moja kwa sifuri na kutinga fainali ya michuano hiyo.