Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili umepewa miezi miwili kujitathimini uwezo wao wa usimamizi wa kutoa huduma na kuboresha huduma kwa wateja.
Hayo yamesema leo Aprili 4, 2022 na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel alipokuwa akizungumza na Viongozi Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya wakijadili kuhusu uboreshaji wa huduma za afya nchini, kikao ambacho kimefanyika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Hapa Muhimbili tunataka huduma kwa wateja ziboreshwe, tunawapa miezi miwili wajipime na kujitathimini uwezo wao wa kutoa huduma bora kwa wateja” Amesema Dkt. Mollel
“Tujiulize swali, watu wengi wanaenda Hospitali binafsi, lakini wakizidiwa wanaletwa Muhimbili na wanapona. Maana yake Wataalam tunao, shida ni ‘Customer Care’ (Huduma kwa Wateja) Amesema Dkt. Mollel
Dkt. Mollel amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kuboresha Sekta ya Afya nchini kwa kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya pamoja na kuhakikisha fedha zinapatikana kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa na vifaatiba na kuongeza kuwa hakuna sababu yoyote ya Watanzania kukosa huduma bora.