Klabu ya Young Africans imethibitisha kurejea kwa kiungo kutoka DR Congo Mukoko Tomombe akitokea nchini kwao.
Tomombe amerejea Tanzania, baada ya dili lake la kujiunga na TP Mazembe kwa mkopo kukwama mwishoni mwa juma lililopita.
Young Africans walidhamiria kumtoa kwa mkopo kiungo huyo, kama sehemu ya kumpata Kiungo Mshambuliaji Chico Ushindi, ambaye tayari ameshatua Jangwani akitokea TP Mazembe.
Tomombe amejiunga na wenzake Jijini Arusha ambapo kikosi cha Young Africans kimeweka kambi ya kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Mzunguuko wa 13 dhidi ya Polisi Tanzania utakaopigwa mwishoni mwa juma hili Mjini Moshi-Kilimanjaro, Uwanja wa Ushirika.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu hiyo Hassan Bumbuli amesema Tomombe amerejea na bado ni mchezaji halali wa Young Africans.
“Mukoko amejiunga nasi hapa Arusha tangu jana, atakuwa sehemu ya kikosi chetu kwa mujibu wa mkataba wake.”
“Taarifa nyingine kuhusu Mukoko zitatolewa baadae lakini ifahamike kuwa bado ni mchezaji wetu,” amesema Bumbuli.
Young Africans leo Jumatano (Januari 19) itacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Mbuni FC katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.
Mbuni FC ni klabu inayoshiriki Ligi Daraja la Pili (First League).