Baada ya mabosi wa Young Africans kumfuta kazi Cedric Kaze, nyota wa timu hiyo Tonombe Mukoko amesema bado wachezaji wana masikitiko ya kufutwa kazi kwa kocha huyo, ila wamepanga kurejesha hali ya ushindi ndani ya timu.

Kaze alifutwa kazi Machi 07 na kocha wake msaidizi Nizar Khalfan kutokana na mwendo mbovu wa timu hiyo katika mzunguko wa pili, hasa baada ya kupoteza 2-1 dhidi ya Coastal Unoin jijini Tanga na kisha kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania jijini Arusha.

Jana Machi 11 Kaze aliwaaga wachezaji wake ambao walionekana wakibubujikwa na machozi kutokana na kocha huyo kutimuliwa akiwa bado hajatimiza malengo yake ya kuwapa ubingwa.

Mukoko ambaye jina lake limetajwa kwenye majina ya wachezaji wa timu ya taifa ya DR Congo amesema kuwa wachezaji pia wana kazi ya kufanya kutimiza majukumu yao kwa ajili ya kuokoa nafasi ya kocha.

“Ikiwa timu inashindwa kupaya matokeo mazuri lawama inakuwa kwa kocha. Lakini na wachezaji pia wana kazi ya kufanya hasa kwa kujituma ndani ya uwanja.

“Wakati wetu ni sasa kutimiza majukumu yetu na kufanya kazi kwa ushirikiano itafanya hata kocha ambaye ataletwa asiwe na kazi kubwa ya kutimiza majukumu yetu.”

Wakati huo huo Uongozi wa klabu ya Young Afrcans umetoa ufafanuzi rasmi kuhusu kocha wa viungo, Edem Mortotsi kutokuwa sehemu ya benchi la ufundi lililovunjwa mwishoni mwa juma lililopita.

Awali Edem alikuwa sehemu ya watendaji wa benchi la ufundi walioondolewa, lakini baada ya majadiliano na uongozi waliona kocha huyo kutoka nchini Ghana aendelee kwa ajili ya kuwapa utimamu wa mwili wachezaji.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Young Africans, Hassan Bumbuli amesema sababu kubwa ya kocha huyo kubakishwa imetokana na kutokuwa na muda wa kutosha kufanya kazi yake, hasa programu yake aliyoiwasilisha kwa viongozi baada ya kuikuta timu ikiwa katikati ya mashindano.

“Suala la kuandaa utimamu wa mwili kwa wachezaji linahitaji muda na utulivu, hivyo kwake yeye hakuwa na muda huo wa kufanya programu zake na uongozi umempa nafasi zaidi”.

Majaliwa azungumzia hali ya Rais Magufuli
Kim Poulsen: Tutaitumia Kenya kutambua udhaifu wetu