Kiungo kutoka DR Congo Mukoko Tonombe amewatuliza Mashabiki na Wanachama wa Young Africans kwa kuwaambia watulie, kwani kikosi chao kipo vizuri na kina malengo makubwa kwa msimu wa 2021/22 ambao utaanza rasmi Mwezi Septemba.
Mukoko ambaye alikua sehemu ya kikosi cha Young Africans kilichocheza dhidi ya ZANACO FC Jumapili (Agosti 29) na kuambuli kibano cha mabao 2-1, ametoa matumaini hayo kwa Mashabiki na Wanachama alipozungumza nao kupitia insta live.
Kiungo huyo aliyesajiliwa Jangwani mwanzoni mwa msimu 2020/21 akitokea AS Vita ya mjini Kinshasa DR Congo, amesema ana uhakika msimu ujao mambo yatawanyookea wakianza na mchezo wa Ngao ya Jamii ambao utapigwa Septemba 25 Uwanja wa Benjanim Mkapa dhidi ya Simba SC.
“Tarehe 12 njooni tena muujaze uwanja maana nyie ndio nguvu yetu. Tupo na Manara tarehe 12 hatoki mtu kwa Mkapa hata ije timu yangu ya Arsenal haitoki, Mpaka kufikia siku ya mechi tutakuwa tumejipanga vyema,” amesema Mukoko
Kuhusu Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika ambapo wataanza na Rivers United ya Nigeria Septemba 12, Mukoko amesema lengo lao kubwa ni kufika mbali na ikiwezekana wacheze hatua ya fainali.
“Malengo yetu kama timu ni kufika fainali ya Klabu Bingwa Afrika na tutahakikisha tunafika.” Ameongeza Mukoko
Kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Young Africans wataanzia nyumbani kupapatuana na Rivers United, kabla ya kwenda Nigeria kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa pili Septemba 19.
Septemba 25 Young Africans itaacheza dhidi ya watani zao wa jadi Simba SC, kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.