Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC Mulamu Ng’ambi amesema, kufuzu Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kuitupa nje CD Primeiro de Agosto ya Angola sio habari sio habari kubwa kwao.
Simba SC ilitinga hatua hiyo Jumapili (Oktoba 16) kwa ushindi wa 1-0, ambao unaifanya klabu hiyo kupata ushindi wa jumla wa mabao 4-1, baada ya kushinda ugenini Luanda-Angola 1-3, Oktoba 09.
Mulamu amesema imekua kawaida kwa Simba SC kucheza hatua ya Makundi ya Michuano hiyo, hivyo wanaona kama wamerejea mahala ambapo wanastahili kuwepo, ili kufanikisha lengo la kufika Nusu Fainali hadi Fainali.
“Kwetu sio stori Simba SC kuingia Group Stage, ni sawa na mtu anaporejea nyumbani kwake, anapofungua mlango huwezi kumsifia kwa kufungua mlango kwa kurudi nyumbani, tumeweza kurudi katika maeneo ambayo tumekuwepo katika miaka hii mitano.”
“Ilitokea mara moja tu, tulishindwa kuingia katika Group Stage katika miaka hii mitano, lakini mara zote tumefanya hivyo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho, kwa hiyo ni muendelezo wetu ambao tumekua tukiufanya katika kipindi hiki.”
“Tunaamini wapinzani wetu wanaiangalia Simba SC imeingia katika hatua hii, wameanza kujiuliza inakuwaje hawa jamaa nao wameingia, kwa hiyo tutahakikisha tunajiandaa ili tukapambane kufikia malengo yetu msimu huu” amesema Mulamu Ng’ambi
Simba SC ilianza Kampeni ya kusaka hatua ya Makundi msimu huu kwa kucheza na Mabingwa Malawi Nyasa Big Bullet na kupata ushindi wa jumla wa 4-0, ikishinda 2-0 nyumbani na ikafanya hivyo ugenini Lilongwe.