Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu kama Mahakama ya Mafisadi, imewahukumu mfanyabiashara Ayoub Kiboko na mke wake Pilly Kiboko kifungo cha miaka 20 gerezani, baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya gramu 251.25 aina ya heroin.

Mahakama pia imeamuru vielelezo ambavyo ni dawa za kulevya viteketezwe, na vielelezo vingine ambavyo ni magari matatu yarudishwe kwa washtakiwa.

Hukumu hiyo imesomwa Desemba 18,2020 na Jaji Mfawidhi, Lilian Mashaka wa Mahakama hiyo, baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi sita wa upande wa mashtaka, upande wa utetezi, vielelezo 16 na sheria na kufikia kutoa hukumu hiyo.

Jaji Mashaka amesema kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka umethibitisha kesi kwa mshtakiwa wa kwanza (Kiboko) wa pili (Pilly) hivyo mahakama inawatia hatiani kwa makosa wanayoshitakiwa nayo ya kusafirisha dawa za kulevya.

Amesema kwa maoni yake utetezi wa washtakiwa  uliunga mkono ushahidi wa upande wa mashtaka kutokana na kujichanganya kwa maelezo yao ya ushahidi walioutoa mahakamani hapo.

Mahakama imezingatia sheria za dawa za kulevya na pia tangu washtakiwa wakamatwe Mei 23, 2018 na muda wote, waliokaa gerezani, hivyo imewahukumu kifungo cha miaka 20 jela na kama hawajaridhika wana haki ya kukata rufaa.

Baada ya washtakiwa kutiwa hatiani, Jaji Mashaka aliwauliza kama wana chochote cha kusema, ambapo Kiboko aliiomba mahakama isiwape adhabu kali licha ya kutiwa hatiani na pia ni shtaka la kwanza kutenda huku Pilly akiiomba mahakama imuhurumie kwa kuwa ana watoto watatu,  ambao hajawaona kwa muda mrefu.

Ruksa hati moja ya ardhi kuwa na majina ya wenza
Armenia yaomboleza wahanga wa Nagorno Karabakh