Hatimaye, Mungu amejibu maombi ya mwanamitindo wa kimataifa Mtanzania, Happiness Millen Magese kwa kumpatia mtoto wa kiume baada ya kilio cha miaka mingi akipigana vita kali na ugonjwa wa endometriosis.
Mrembo huyo ambaye alishinda taji la Miss Tanzania mwaka 2001 ame-share na dunia habari njema na furaha yake kupitia mtandao wa Instagram akimshukuru Mungu kwa kumpa baraka aliyokuwa akimuomba kwa muda mrefu.
Mrembo huyo ameandika ujumbe kwa mwanae akimtaka kuwa baraka, matumaini na muujiza kwa mamilioni ya wanawake duniani wanaotamani kupata watoto lakini wameshindwa kutokana na kuwa na ugonjwa huo.
“Ukalete matumaini, imani na miujiza kwa mamilioni ya wanawake duniani wanaotamani kubeba watoto wao kama nilivyokuwa nikitamani kukubeba wewe. Ukue na kuibadili dunia kwa ajili ya wengine. Ukamuamini Mungu na kumiliki miujiza yake,” ameandika mrembo huyo.
- LIVE: Ziara ya Rais Magufuli mkoani Kigoma
- Mamilioni wajiunga na maandamano Venezuela, yasababisha vifo
“Kwa kadiri ambavyo maisha yanaweza kuwa magumu, ujifunze kuwa mvumilivu, ufanye kazi kwa bidii na ukijua kuwa kila kitu wakati wote hutokea kwa sababu na kila binadamu ana njia yake na Mungu ana mpango kwao,” aliongeza.
Millen Magese aliweka wazi kuwa mtoto huyo anampa jina la baba yake mzazi, akieleza kuwa hatimaye amempata baba yake.
Kwa miaka mingi, Millen Magese amekuwa akisumbuliwa na endometriosis, na aliamua kuanzisha harakati za kuwasaidia wanawake wanaosumbuliwa na ugonjwa huo duniani kote hususan Afrika.
Amekuwa mstari wa mbele kutoa msaada kwa mashirika yanayojihusisha na kutoa huduma za kujitolea kwa umma hususan matatizo ya uzazi kwa wanawake.
Ujumbe wa Magese utaifikia dunia nzima kwa urahisi kwani ni mrembo aliye chini ya makampuni makubwa ya mitindo kama Ford Models la New York Marekani na Ice Mode Management la Afrika Kusini, na amekuwa akipewa nafasi na vyombo vya habari vya kimataifa kama CNN.
Dar24 inampongeza Millen Magese kwa kupata mtoto wa kiume. Mungu ambariki.