Serikali imedhamiria kubadilisha muonekano wa majiji yote hapa nchini ili yawe na barabara za viwango vya kimataifa na zinazopitika kwa urahisi ili kuepukana na msongamano.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alipokuwa akizungumza na wananchi wa Tengeru, wilayani Arumeru, mkoani Arusha mara baada ya kukagua barabara ya Sakina-Tengeru yenye urefu wa km. 14.1 ambayo itakuwa na njia nne za magari.
“Tumeanza kujenga barabara za kisasa katika jiji la Arusha ambalo ni jiji la utalii, tutakwenda Mwanza na Dar es Salaam kwa kujenga barabara zenye njia za juu (flyovers) zikiwemo za magari na za waenda kwa miguu,”amesema Majaliwa.
Aidha, Majaliwa amesema kuwa uboreshwaji wa barabara hizo utasaidia wafanyabiashara kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi na viwanda vitakapoanza kujengwa, itakuwa hawana shida ya mawasiliano.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Eng. Mgeni Mwanga amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ambao ulianza Juni 2015, unatarajia kukamilika Juni 2018.
Naye mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari amesema uhaba wa ardhi bado ni tatizo kubwa kwenye wilaya hiyo kiasi kwamba hawana hata eneo la kujenga shule au zahanati.