Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imekutana na wadau kutengeneza Mwongozo wa Taifa wa uendeshaji wa Mabaraza ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa na familia wenye lengo la kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa Mabaraza hayo nchini.

Akizungumza katika kikao hicho mkoani Morogoro Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii Baraka Makona amesema, lengo la kikao hicho ni kupata maoni ya wadau katika kuuboresha Mwongozo huo ili uendelee kutatatua migogoro mbalimbali inayotokea katika ndoa na familia.

“Ndoa na familia nyingi zimekuwa zikikumbwa na migogoro inayosababisha mtengano wa familia hasa watoto kukosa malezi na makuzi na wengi wao kuishia kufanya kazi na kuishi mitaani” alisema Baraka

Akiongea katika Kikao hicho, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwajuma Lukindo, amesema Mwongozo huo utasaidia kuelekeza namna ya kufuata pale migogoro ya ndoa na familia inapofika katika ngazi ya mahakama kwa kufuata njia maalum kwa kutumia mfumo wa kupokea taarifa kutoka katika Mabaraza hayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii Dkt. Joyce Nyoni amesema Mwongozo huo utasaidia Wanandoa na familia kutatua changamoto zao, hivyo ukitekelezwa itasaidia kurudisha uhusiano katika ndoa na familia na sio kuvunjika kwa mahusiano hayo.

Naye Afisa wa Jinsia kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Getrude Diabele amesema Shirika hilo linashirikiana na Wizara kuhakikisha kunakuwa na Uratibu mzuri wa uendeshaji wa Mabaraza ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa na familia katika jamii ikiwemo Usawa wa Kijinsia katika Mabaraza hayo ambayo mengi yao yana wajumbe wa jinsi ya kiume pekee.

“Wadau tutaendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha Mwongozo huu unatekelezeka ili kuyapa Mabaraza ya Usuluhishi wa Migogoro ya ndoa na Familia uwezo wa kusuluhisha migogoro hiyo kwa ngazi ya Familia na Kata bila kufikia hatua za talaka” alisema Getrude

Kwa upande wake Katibu wa Kadha Mkuu wa BAKWATA Hamis Kwangaya  amesema Mwongozo huo utaisaidia Taasisi hiyo kuongeza mbinu katika Baraza la usuluhishi wa migogoro ya Ndoa na familia lililopo katika Taasisi hiyo kufanya kazi kwa ufanisi na kutatua migogoro hiyo katika jamii.

Baraza la Usuluhishi wa Ndoa la Kamishna wa Ustawi wa Jamii ni chombo cha Serikali kilichoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa Na.5 ya mwaka 1971 na kutangazwa na Waziri wa Katiba na Sheria katika Gazeti la Serikali Na.196 la mwaka 1971.

Baraza la Ndoa la Kamishna wa Ustawi wa Jamii liliundwa ili liweze kushughulikia migogoro ya Ndoa kwa Watanganyika wote bila kujali itikadi zao za dini,kabila, jinsia au dhehebu.

Baraza la Usuluhishi wa Ndoa la Kamishna wa Ustawi wa Jamii ni la kipekee kwa muundo na ufanyaji wake wa kazi ukilinganisha na Mabaraza mengine yanayoshughulikia migogoro ya Ndoa ambayo yanaendana na mila na desturi zao mfano Imani za dini, kabila, dhehebu na eneo mhusika anapoishi(kata)

Sensa ya watu na makazi yabadili kalenda ya mihula
Waziri Jafo aagiza wadau kuzingatia takwimu za hali ya hewa