Mwenyekiti wa Klabu Simba SC Murtaza Mangungu amewataka Watanzania kutambua na kuthamini mchango uliotolewa na klabu hiyo katika Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.

Mangungu ametoa kauli hiyo katika hafla maalum ya uzinduzi wa Kampeni ya Kuhamasisha Wanachama na Mashabiki wa Simba SC kwenda Uwanja wa Benjamin Mkapa kuishangilia timu yao, kwenye mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho, dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini, Jumapili (April 17).

Kiongozi huyo amesema: “Nchi ambazo zimeingiza timu Robo Fainali hazizidi tano, kuna watu wanajifanya hawaoni jitihada ambazo zimefanywa na Simba. Mwakani Tanzania tutaingiza tena timu nne kwenye mashindano ya CAF na hizi ni jitihada za Simba.”

Katika hatua nyingine Mangungu amewahakikishia Mashabiki na Wanachama wa Simba SC kuwa, timu yao ina kikosi kizuri na imejiandaa kwenda kupambana kwa dakika 180 za Robo Fainali kwa lengo la kusaka ushindi na kusonga mbele.

“Niwahakikishie Wanasimba na wapenzi wa soka, leo hii tunaenda kucheza mchezo kwa dakika 180 (Nyumbani na Ugenini) kutafuta nafasi ya kucheza nusu fainali sababu tuna wachezaji ambao wanajitambua, tuwaombee wafanye vizuri.” amesema Mangungu

Simba SC ilitinga Robo Fainali kwa kishindo kwa kuichapa USGN ya Niger mabao 4-0 kwenye mchezo wa Hatua ya Makundi, ikimaliza nafasi ya pili kwa kufikisha alama 10 sawa na RS Berkane ya Morocco.

Uongozi Simba SC wapokea ombi la Mzee Dalali
Hassan Dalali: Tupeni nafasi tuzungumze na wachezaji