Watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Uganda wamewasha moto wakidai kuwa kuna upendeleo wa kisiasa katika ugawaji wa vibali vya kufanya matamasha ya muziki nchini humo, baada ya kuzuia tamasha la Bobi Wine huku Ikulu ikiunga mkono tamasha la Bebe Cool.
Wasanii hao walikuwa na ratiba ya kufanya yao jana ikiwa ni siku ya Boxing Day. Polisi wameeleza kuwa Bobi Wine hakuruhusiwa kufanya tamasha lolote la muziki kwakuwa amekuwa akikiuka taratibu na kwamba hata tamasha aliloliandaa halikuombewa kibali rasmi.
“Tutakuwa Busabala Beach (Bobi Wine alipopanga kufanya tamasha), na tutawatawanya wote watakaofika kwa sababu tunawalinda. Kwa jinsi ninavyofahamu, tamasha hili halikufuata utaratibu kwa sababu mambo mengi hayajakamilishwa,” msemaji wa Polisi, Emilian Kayima alisema awali.
-
Kigwangalla aibukia sakata la Fastjet kunyimwa vibali
- Hofu yatanda wakimbia makazi yao kwa kukosa choo
Bobi Wine ambaye ni mbunge na mkosoaji mkubwa wa Serikali ya Rais Yoweri Museveni, aliandika kupitia Twitter akielezea jinsi ambavyo tamasha lake hilo lililokuwa limepangwa kufanyika ‘One Love Beach Busabala’ katika maeneo ya Kampala lilivyovamiwa na Polisi.
“Hivi sasa makumi ya askari polisi wamezunguka eneo la One Love Beach Busabala ambako tamasha letu linapangwa kufanyika kwa ajili ya Boxing Day. Baadhi ya wafanyakazi wamekamatwa, mafundi mitambo wameambiwa wafungue kila kitu, kinyume cha maagizo ya Bunge,” alitweet Bobi Wine.
Bunge la Uganda liliamuru Jeshi la Polisi kuhakikisha halizuii matamasha ya Bobi Wine likieleza kuwa ni kinyume cha Katiba ya Nchi.
Wakati huohuo, video ya Rais Museveni akiunga mkono tamasha la Bebe Cool ambaye ni hasimu wa Bobi Wine na msanii anayeunga mkono Serikali imesambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Katika kipande hicho cha video, Rais Museveni anamwambia Bebe Cool kufanya muziki ambao unalenga kuleta maendeleo nchini humo, na pia akawatakia kila la kheri watu watakaohudhuria tamasha hilo.
Hatua hiyo imetafsriwa na wengi kama upendeleo wa kitofauti kwa wasanii hao ambao wamekuwa washindani wakubwa kwa muda.