Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), amekataa kuahirisha kikao cha ishirini cha viongozi wa jumuiya hiyo jijini Arusha, baada ya Burundi kumtaka kufanya hivyo.
Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, anataka kikao hicho kiahirishwe kwa wiki mbili zaidi, akisema kuwa Burundi haijajitayarisha kushiriki mkutano huo.
Aidha, ajenda kuu ya mkutano huo ni mzozo wa kisiasa wa Burundi, baada ya wawakilishi wa serikali kukosa kushiriki mazungumzo ya amani yaliyo kuwa yakiongozwa na rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa jijini Arusha nchini Tanzania.
Hata hivyo, Rais wa Uganda Yoweri Museveni amependekeza kwamba Burundi inastahili kujipatia katiba mpya, itakayo jumuisha maoni ya kila mwananchi na kuruhusu raia wake wote waliokimbilia nchi za nje kurejea nyumbani.