Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amewaomba radhi wakenya kwa machapisho ya mtoto wake aliyoyatoa siku ya Jumatatu na Jumanne (Octoba 3-4, 2022), kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter.
Kupiti taarifa aliyoitoa hii leo Oktoba 5, 2022 Rais Museveni amesema amesikitishwa na kitendo hicho na kuwaomba Wakenya msamaha huku akisema maafisa wa umma wa kiraia au wa kijeshi, haipaswi kuingilia masuala ya udugu wa taifa moja na jingine.
Amesema, “Nawaomba ndugu zetu wa Kenya watusamehe kwa alichoandika kwenye twitter, alichofanya aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Nchi Kavu hapa, (Jenerali Muhoozi), si sahihi kwa maafisa wa Umma, wawe wa kiraia au wa kijeshi, kutoa maoni yao au kuingilia kwa njia yoyote ile, katika mambo ya ndani ya nchi ndugu.”
Mtoto huyo mkubwa wa Museveni, Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, alituma ujumbe ‘tata’ kwenye mtandao wa Twitter siku ya Jumatatu, na kuibua hasira ya Wakenya wengi mtandaoni ambapo aliandika kwamba itamchukua yeye na jeshi lake wiki mbili kuuteka mji mkuu wa Nairobi.
Kauli hiyo, iliyoibua hasira kwa Kenya na mjadala mkubwa katika nchi za Afrika Mashariki na katika ujumbe wake mwingine, akaandika kuwa, alisikitishwa na aliyekuwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kwa kutowania muhula mwingine wa urais, wakati angeweza kushinda uchaguzi kirahisi.
Hapo jana, (Oktoba 4, 2022), Rais Museveni alimfuta kazi Jenerali Kainerugaba kama kamanda wa vikosi vya nchi kavu lakini akampandisha cheo cha juu zaidi cha jeshi na kusema amefanya hivyo kwakuwa Jenerali Kainerugaba alikuwa ametoa mchango mkubwa kwa nchi hiyo na bado angeweza kufanya hivyo.