Chama cha wachezaji wa soka nchini SPUTANZA, kimetangaza kukubalina na maamuzi yaliyofikiwa na kamati ya nidhamu ya shirikisho la soka TFF, ambayo imetangaza maamuzi ya kuwafungia maisha na kwa muda wa miaka kumi baadhi ya viongozi na wachezaji wa klabu za ligi daraja la kwanza.

Mwenyekiti wa SPUTANZA Mussa Kisoky, amesema kwa kuwa kamati imejiridhisha na ushahidi uliotolewa na wale walioitwa kuhojiwa, hapana shaka yeyote kuwa adhabu hizo sahihi ingawa nyingine zimepunguzwa makali.

Amesema kama mtu amebainika kuhusika katika zoezi la kupanga matokeo adhabu yake ni kifungo cha maisha asijihusishe na soka, lakini kitendo cha kamati kuwafungia kutojihusisha na soka kwa kipindi cha miaka kumi na kutakiwa kulipa faini ya shilingi milioni kumi ni sawa na kuwapunguzia adhabu wahusika waliokutwa na makosa.

“Unajua adhabu iliyotolewa ya kuwafungia miaka kumi na kuwalipisha faini, kamati imewahurumia sana ilitakiwa wafungwe kifungo cha maisha kwa mujibu wa kanuni”

“Lazima ifahamike kwamba soka letu linaongozwa na kanuni ambazo tumekubaliana sisi wenyewe wahusika wa mpira wa miguu, sasa akitokea mtu akaivunja kwa makusudi ni lazima ahukumiwe.” Alisema Kisoki.

Kamati hiyo chini ya mwenyekiti wake Abbas Talimba, iliwahukumu kifungo cha maisha na wengine kutojihusisha na soka kwa kipindi cha miaka kumi na kutakiwa kulipa kiasi cha shilingi milioni kumi kila mmoja baada ya kuwabaini kuhusika katika kashfa ya upangaji matokeo iliyohusisha michezo ya kundi “C” katika ligi daraja la kwanza.

Miongoni mwa waliofungiwa ni pamoja kutojihusisha na soka ni mwamuzi wa mchezo kati ya JKT Kanembwa FC v Geita Gold, Saleh Mang’ola na kamisaa wa mchezo huo Moshi Juma baada ya kukutwa na hatia ya upagaji matokeo.

Aidha kamati pia imemkuta na hatia kocha msaidizi wa klabu ya Geita Gold, Choke Abeid na kumfungia maisha kutojihusisha na mpira wa miguu

Magolikipa Mohamed Mohamed wa JKT Kanembwa na Dennis Richard wa Geita Gold wamefungiwa miaka 10 kutojihusisha na mpira wa miguu sambamba na kulipa faini ya shilingi milioni kumi (10,000,000) kila mmoja.

Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Geita (GEREFA), Salum Kurunge, Mwenyekiti wa klabu ya Geita Gold, Cosntantine Moladi na Katibu wa klabu ya JKT Kanembwa Basil Matei wameachiwa huru na Kamati ya Nidhamu baada ya kutokutwa na hatia katika shauri hilo.

Mwenyekiti wa chama cha mpira wa miguu mkoa wa Tabora, Yusuph Kitumbo, Katibu wa chama cha mpira wa miguu mkoa wa Tabora, Fateh Remtullah, Mwenyekiti wa klabu ya JKT Oljoro, Amos Mwita na kocha msaidizi wa Polisi Tabora, Bernad Fabian wamefungiwa maisha kutojihusisha na mpira wa miguu.

Mwamuzi wa mchezo kati ya Polisi Tabora v JKT Oljoro, Masoud Mkelemi na mwamuzi wa akiba, Fedian Machunde wamefungiwa kwa muda wa miaka kumi kutojihusisha na mpira wa miguu, na kutozwa faini ya shilingi milioni (10,000,000) kumi kila mmoja.

Katibu wa klabu ya Polisi Tabora, Alex Kataya, Katibu wa klabu ya JKT Oljoro, Hussein Nalinja, mtunza vifaa wa klabu ya Polisi Tabora, Boniface Komba, na Meneja wa timu ya  Polisi Tabora, Mrisho Seleman, wameachiwa huru na Kamati ya Nidhamu ya baada ya kutokutwa na hatia.

Klabu za Geita Gold (Geita), JKT Oljoro (Arusha) na Polisi Tabora (Tabora) zimekutwa na hatia ya upangaji wa matokeo na kupewa adhabu ya kushushwa daraja mpaka ligi daraja la pili (SDL) msimu ujao.

Upande wa klabu ya JKT Kanembwa FC ya mkoani Kigoma, imeshushwa daraja mpaka kwenye ngazi ya ligi ya mkoa (RCL), baada ya kushika nafasi ya mwisho katika msimamo wa kundi lake, Kundi C.

Kutokana na maamuzi hayo ya Kamati ya Nidhamu ya TFF, Kamati husika zitakaa kupitia Kanuni na kutangaza timu itakayopanda Ligi Kuu (VPL) msimu ujao na timu zitakazopanda Ligi Daraja la Kwanza (StarTimes) msimu ujao.

Antonio Conte Ajivisha Kitanzi Kilichomnyonga Mourinho
Mrema apigwa chini Mahakamani, Akubali Kumlipa Mbatia