Gwiji wa Soka nchini Morocco Mustapha Hadji, anaamini Kocha Mkuu wa timu ya Taifa hilo Walid Regragui, bado ana nafasi ya kuishangaza Dunia, baada ya kufanya ivyo kwa kuzitoa Hispania na Ureno kwenye Fainali za Kombe la Dunia zinzoendelea nchini Qatar.
Morocco leo Jumatano (Desemba 14) itacheza kwa mara ya kwanza Mchezo wa Nusu Fainali wa Fainali hizo, baada ya kuvunja Rekodi za Cameroom, Ghana na Senegal, ambazo ziliwahi kuishia hatua ya Robo Fainali.
Mustapha Hadji ambaye aliwahi kutamba na Kikosi cha Morocco katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1994 na 1998 amesema, anaamini Taifa lake lina uwezo wa kupambana na yoyote na kupata matokeo ambayo yataendelea kuishangaza Dunia.
“Nina imani kubwa na Timu yangu kufanya maajabu zaidi katika Fainali za Kombe la Dunia, haitoshi kusema walipofikia inatosha, ninaiona nafasi ya kutinga Fainali na ikiwezekana kutwaa Ubingwa wa Dunia, ili Afrika na Morocco ziheshimike.”
Katika hatua nyingine kiungo wa zamani na Kocha Msaidizi, amempongeza Kocha Walid Regragui, kwa kazi nzuri aliyoifanya tangu alipokabidhiwa jukumu la kukinoa Kikosi cha Morocco, akichukua nafasi ya Kocha Vahid Halilhodzic.
“Ni miezi miwili au mitatu tu tangu Walid Regragui awasili katika timu ya taifa. Kulikuwa na mzozo na Vahid.”
“Kocha mpya aliweza kupata maneno na njia ya kuwatoa wachezaji bora na kutengeneza timu yenye ari kubwa. Na timu inacheza kwa moyo na hali ya juu.” amesema Hadji ambaye alikua Kocha msaidizi kuanzia mwaka 2014 hadi mapema mwaka huu.
Morocco itacheza dhidi ya Ufaransa katika mchezo wa Nusu Fainali ya Pili leo Jumatano (Desemba 14), Mshindi wa mchezo huo atakutana na Argentina iliyotangulia Fainali baada ya kuichakaza Croatia jana Jumanne (Desemba 13) kwa mabao 3-0.